Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani Philiberto Sanga amewataka viongozi wa Vyama vya Msingi ( AMCOC ) kuzingatia miongozo ya utekelezaji wa Mfumo wa Stakabadhi Gharani ili kuepukana na sintofahamu kwa wakulima wa zao la Korosho kama ilivyotokea katika msimu uliopita.
Akifungua mafunzo kwa vyama hivyo leo katika ukumbi wa Parapanda Mkuranga Sanga aliwataka washiriki kuwa makini na mafunzo hayo na kuwataka kuyafanyia kazi na hatimaye uwe mwarobaini wa kumaliza changamoto mbambali kwa wakulima wa zao la Korosho.
Sanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye aliwakilishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mhandisi Mshamu Munde alitumia fursa hiyo kuwaonya viongozi hao kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atayekwamisha malipo ya korosho kwa wakulima katika msimu huu.
Pamoja na hayo alisisitiza zaidi kwa kuwageukia walanguzi wa korosho “Kangomba” kwamba watafute kazi nyingine ya kufanya ili kuepukana na mkono wa sheria kama ambavyo Rais Dkt John Pombe Magufuri ameagiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Halmashauri Julita Bulali pamoja na kuipongeza Benki ya NMB Tawi la Mkuranga kwa kudhamini mafunzo hayo aliwataka viongozi hao wahakikishe mfumo unawanufaisha wakulima , Halmashauri na Serikali kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Juma Abeid akifunga mafunzo hayo, aliwataka viongozi wa vyama hivyo kutenda haki kwa wakulima huku akiwaagiza makatibu wasifanye kazi kwa mazoea ili kuepuka taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa ( TAKUKURU ) Mkuranga, kuwachukulia hatua kwani wao watazingatia sheria , taratibu na kanuni, pia amemshauri Mrajisi Msaidizi Mkoa wa Pwani ikiwezekana kuwaondoa Makatibu wote waliovuruga msimu uliopita na waajiriwe makatibu wengine wenye sifa.
Mafunzo haya yanafanyika ikiwa ni mkakati wa kulifanya zao hilo la Korosho linakuwa na thamani kubwa na hasa ukilinganisha na umuhimu wake kwani ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.