Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo ameziagiza Kamati zote za Ulinzi na Usalama za Wilaya Mkoani Pwani kuwachukulia hatua watu wote watakaogundulika kufanya ubadhilifu kwa wakulima wa Korosho na kuzitaka kamati hizo kumpa taarifa za utekelezaji huo ndani ya siku saba.
Akifungua Mkutano wa wadau wa Korosho Mkoa wa Pwani uliofanyika katika ukumbi wa Flex Garden Kiguza Wilaya ya Mkuranga Ndikilo amezitaka taasisi zote za fedha zilizoshiriki katika kufanya malipo kwa wakulima wa Korosho kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama za Wilaya ili kubaini kasoro zilizosababisha baadhi ya wakulima kutopata fedha zao
Aidha amempongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kufanya maamuzi ya busara kwa kununua korosho zote msimu wa 2018/2019 na kusema hadi sasa Serikali imeshafanya malipo kwa wakulima wa Korosho kiasi cha shilingi Bilion 47.7 na kubaki kiasi cha shilingi bilioni 18.1 ambazo wakulima hawajalipwa.
Ndikilo amewahakikishia wakulima wa zao hilo Mkoa wa Pwani kuwa Korosho zote zilizokusanywa na Serikali zimeshauzwa na kuwataka wawe na subila ili kuona Serikali inamalizia kuhakiki mapungufu yaliyopo ili kila mkulima aweze kupata fedha zake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga akijibu swali kwa wadau wa Mkutano huo wa Korosho amesisitiza kwa upande wa Wilaya ya Mkuranga hatovifumbia macho Vyama vya Msingi au viongozi wa Vyama hivyo na kuahidi kuwachukulia hatua kali wale wote walioshiriki kufanya ubadhilifu sambamba na kurudisha fedha na hata kuvifuta baadhi ya vyama vya Msingi ambavyo vitaonekana havina tija kwa wakulima wa Korosho Wilayani humo.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho (CBT) Francis Alfred amesema wao kama bodi ya korosho wanaahidi kutoa mafunzo kila kijiji ndani ya Mkoa wa Pwani katika zao la Korosho ili kuifanya korosho ya Pwani inakuwa na ubora kama ilivyo mikoa mingine.
Chama kikuu cha ushirika mkoa wa pwani (CORECU) kimetakiwa kuandaa magunia mapema sambamba na maghala ili kujiandaa na msimu wa mwaka 2019 – 2020 huku wakulima wakitakiwa kutochanganya Korosho na michanga au takataka zozote kwa lengo la kuongeza uzito.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.