Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani Filberto Sanga ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama sambamba na watendaji wa vijiji kuhakikisha wanatokomeza kabisa ubakaji na ulawiti dhidi ya watoto.
Akizungumza na wananchi kwenye kilele cha siku ya mtoto wa afrika ambayo kiwilaya ilifanyika kwenye kijiji cha Bupu mwishoni mwa wiki, Sanga alizigeukia mahakama na Jeshi la Polisi akizitaka kuharakisha upelelezi na kutoa hukumu mara moja kwa wote watakaokutwa na hatia ya ubakaji na ulawiti
Aidha kiongozi huyo aliwataka wazazi na walezi kuhamasishana na kuunda kamati itakayoratibu michango ya pesa na vyakula kwenye vijiji vyote (125) hatimae watoto wapate milo shuleni ili kuchochea kiwango cha ufaulu sambamba na kupunguza utoro.
Sanga alitumia fursa hiyo kumpongeza mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mhandisi Mshamu Munde, Asasi za kiraia na wadau wa maendeleo kwa mikakati yao ya kuhakikisha mtoto ambaye ni msingi wa Taifa endelevu anapata ulinzi ,matunzo,sambamba na kumwendeleza huku akiagiza idara ya maendeleo ya jamii kusambaza taarifa yao kwenye vitongoji na viiji ili iwe agenda ya kudumu kwenye vikao vyao.
Awali Mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii Halmashauri ya Wilaya Peter Nambunga pamoja na kuwashukuru waliochangia sherehe hizo akiwemo Ahmed Salum aliomba serikali kuongeza adhabu kwa wabakaji na kutenga gereza lao wakiwa na sare zenye majina “walawiti” kutangazwa ili jamii iwafahamu.
Hafla hiyo iliambatana na burudani mbali mbali ikiwemo ngoma ya sindimba na bunge la watoto ambavyo viliwakuna mno wananchi.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.