Naibu Waziri,Wizara ya Madini Mh Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wote wa madini ya ujenzi kufuata sheria pindi wanapopewa leseni za uchimbaji wa madini hayo katika maeneo waliyopewa.
Mh Nyonge aliyasema hayo hapo jana wakati alipofanya ziara kwenye Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani ambapo alitembelea katika kiwanda cha kutengeneza marumaru (Goodwill Ceramic Tanzania Limited) pamoja na kiwanda cha Neelkant Salt ambapo pia alitembelea kwenye mashamba ya chumvi katika kata ya Shungubweni.
Mh Nyonge aliongeza kwamba”Mtu anayepewa leseni ya kuchimba madini ya mchanga lazima afuate sheria, anatakiwa aonyeshe namna atakavyolinda maeneo ya uchimbaji na kama hatafuata sheria atachukuliwa hatua”
Mh nyonge alisisitiza”kama mtu hana leseni ya kuchimba madini ya ujenzi hataruhusiwa kuchimba”.
Afisa Mazingira Wilaya Bwana Herman Basisi anasema kuna changamoto kubwa kwa wachimbaji wa mchanga ambapo hawashirikishi Halmashauri pindi wanapoomba leseni za uchimbaji wa mchanga na matokeo yake Halmashauri inakuja kugundua baadae wakati uchimbaji umefanyika bila taratibu kufuatwa na mazingira kuharibiwa.
Basisi anaongeza kwamba wachimbaji kutopitia Halmashauri wanasababisha migogoro kati ya majirani wa eneo la uchimbaji kutokana na kuingiliwa kwa maeneo yao hii inatokana na kukosa ushauri kutoka kwa wadau wa mazingira kama ofisi ya Mazingira na Ardhi.
Wakati huo huo Naibu Waziri huyo ametoa agizo kwa kampuni ya RAK inayochimba madini ya chaoline katika Wilaya ya Kisarawe kusitisha machimbo hayo mpaka hapo Wizara ya Madini na TRA kufanya mahesabu.
“Kampuni ya RAK wachimbaji wa madini ya
chaolin nimewazuia kufanya kazi mpaka hesabu zikae sawa na vilevile TRA pamoja na Wizara yangu wapige hesabu na hesabu ikishajulikana watulipe hesabu yetu ili serikali ipate kiwango ambacho inastahili kupewa” Nyongo alisisitiza
Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga imefanikiwa kutenga maeneo saba rasmi ya uchimbaji wa mchanga ambayo yapo vijiji vya Magodani, Vianzi, Dondo, Binga,Dondwe,Mkiu na Lukanga ili kunusuru uchimbaji holela ndani ya Halmashauri na kuepusha uharibifu wa Mazingira.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.