Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga jana imeadhimisha siku ya upandaji miti kiwilaya ambapo ilifanyika katika kijiji cha mlamleni kata ya Tambani ambapo wananchi wa kijiji hicho wamefanikiwa kupanda jumla ya miti 1500 ambapo miti mingine imepandwa kwenye shule za sekondari na shule za msingi,chuo cha ualimu vikindu,watu binafsi, Taasisi,msitu wa hifadhi wa vikindu.
Akizungumza katika zoezi hilo la upandaji miti,Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mh.Filberto Sanga alisema miti ina kazi kubwa kwani inatusaidia kupata nishati ambayo hutegemewa na sehemu kubwa ya watanzania kama vile kuni na mkaa,husaidia kupata malighafi za viwanda vya dawa na mbao,hutunza mazingira,hutunza vyanzo vya maji,majengo na huzuia mmomonyoko wa ardhi.
Mh Sanga aliongeza kwamba kila mwananchi lazima ashiriki kupanda miti angalau miti kumi kila mwaka na taasisi kama vile shule zinazotumia kuni kuandaa chakula zinatakiwa kuwa na mashamba ya miti,vijiji na watu binafsi wanatakiwa kuwa na misitu kwani kwa kufanya hivyo itaboresha hali ya mazingira na kuboresha hali ya hewa kwa kupata mvua kwa wakati muafaka.
Mh Sanga amewaonya wananchi wote wanaofanya shughuli zisizokubalika za kuharibu misitu kama vile kulima, kukata miti na kuchoma mkaa ama kwa makusudi ama kwa kutojali umuhimu wa msitu.
Afisa Mtendaji kata ya Mlamleni bwana Abbas Likonda ameahidi kulitunza eneo lilipandwa miti kwa kushirikina na wananchi wa kijiji hicho.
Aidha bwana Likonda aliongeza kwamba elimu ya utunzaji wa misitau itakuwa ajenga ya kuduma kwa kila mkutano wa kijiji na kata ili wananchi wasiende kinyume na utaratibu waliojiwekea katika utunzaji wa miti.
Mwenyekiti wa vijana kijiji cha Mlamleni bwana Sudi Matimbwa alisema “tunashukuru vijana tumepewa eneo la kufanya mazoezi ambalo lipo jirani na eneo tulilopanda miti,tunaahidi kila tunapokuja kufanya mazoezi tutakagua miti na baadae kufanya mazoezi ili kuhakikisha miti tuliyoipanda leo hii inakua vizuri”
Maamuzi ya kupanda miti kila mwaka yamefikiwa baada ya kuona misitu katika nchi yetu inazidi kutoweka kutokana na shughuli za kila siku za kibinadamu na hasa matumizi yanayozidi kiwango cha uwezo wa misitu yetu kujizalisha.
Aidha juhudi endelevu zinazofanyika za kurudishia uoto wake asili ni kidogo kulingana na kiwango cha uvunaji,hali hii imesababisha maeneo mengi kukosa miti na kunyemelewa na jangwa,kupata athari za mabadiliko ya tabia ya nchi kama vile mabadiliko ya hali ya hewa, mafuriko, joto kali, mmomonyoko wa udongo,upotevu wa aina nyingi za mimea na kukauka kwa vyanzo vya maji.
Ili kurekebisha na kupambana na athari hizo,taifa limeagiza kila wilaya kupanda miti milioni moja laki tano (1,500,000) kila mwaka katika maeneo mbalimbali hasa katika vyanzo vya maji ambavyo vimekwisha haribiwa na maeneo yaliyowazi bila miti au uoto asili.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.