Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Bwana Peter Nambunga amewataka wananchi wa Mkuranga kupunguza tatizo la lishe duni.
Nambunga aliyasema hayo hapo jana wakati wa kikao cha kawaida cha robo cha kamati ya lishe Wilaya ambapo alisema ”pamoja na juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau kuendelea kupambana na lishe duni takwimu zinaonyesha kuwa na upungufu wa damu unaendelea kuwa juu kwa wanawake waliokuwa katika umri wa kuzaa wapo asilimia 45, watoto chini ya miaka mitano wana upungufu wa damu asilimia 58 wakati uzito pungufu kwa wajawazito ni asilimia 16-30, watoto chini ya miaka mitano uzito wao ni pungufu zaidi ya asilimia 50 na Utapiamlo mkali ni kuanzia asilimia 5-8 na udumavu ni asilimia 30.
Nambunga aliongeza kwamba Wilaya ya Mkuranga inalima vyakula mbalimbali na vingi inachotakiwa ni wananchi wapewe elimu ya namna ya ulaji wa vyakula hivyo ili kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la lishe duni.
Afisa lishe Wilaya Bi. Vumilia Ngandago alisema waathirika wa lishe duni ni makundi yote ya binamu ambapo ni watoto chini ya miaka mitano, vijana, wajawazito, wanaonyonyesha na wazee.
Ngandago aliongeza kwamba dalili za lishe duni ni upungufu wa damu, ukosefu wa vitamin A ,ukosefu wa madini joto, uzito pungufu, Utapiamlo mkali na udumavu.
Ngandago alibainisha baadhi ya sababu za lishe duni katika wilaya ya Mkuranga ambapo ni uelewa mdogo wa jamii, kamati na wataalam juu ya ulaji sahihi, kutokuwa na chakula cha kutosha chenye virutubishi muhimu, kutokuwa na mpango wa chakula mashuleni, mila na desturi ya jamii ya jamii ya Mkuranga, hali duni ya uchumi yaani jamii kubwa ya mkuranga wana kipato kidogo chini ya 2000.
“Tumejipanga kutoa elimu kuanzia ngazi ya wilaya, kata mpaka vijiji kwani tukiwaelimisha na wao watasaidia kuelimisha kwenye vikao mbalimbali katika maeneo yao kuhusu lishe na hivyo kupunguza unasihi wa lishe.”Ngandago alisema
Mhe. Hassan Dunda Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji na Diwani wa kata ya Mkamba alisisitiza kwa kusema kwamba wataalam wahusike kuwasaidia wananchi kuhusu suala la lishe kwa kutoa elimu kuanzia ngazi za vijiji hadi kata kwa kutumia maonesho ya sinema ambazo zinaonyesha athari za lishe duni na namna ya kula vyakula bora ambavyo vitaondoa tatizo hilo.
Faviana Mlaki mdau wa lishe kutoka asasi ya Jipeni Moyo Women Community Organization(JIMOWACO) alisema” asasi yetu itasaidiana na Halmashauri ili kutekeleza suala la lishe vizuri kwakua tunatekeleza mradi kupitia watoa ushauri katika ngazi za vijiji na kaya hivyo tutawaelimisha kuhusu lishe na wao wataenda kwenye kila kaya kutoa elimu hiyo ili kuondoa kabisa tatizo la lishe duni katika wilaya yetu.”
Kikao hicho kiliibuka na mikakati mbalimbali ya namna ya kuepuka na kuondokana na hali duni ya lishe kwa kuendelea kutoa tiba, kuelimisha jamii kuhusu masuala ya lishe kwenye sekta mbalimbali, kuendelea kuomba wadau waliopo wasaidie kuhamamisha na kutoa elimu, kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa sawasawa na viashiria vilivyopangwa na kamati ya lishe wilaya kila mmoja kwa nafasi yake awajibike kutoa elimu, na kutoa elimu kupitia redio, sinema, vipeperushi na majarida.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.