Wananchi wa kijiji cha Hoyoyo katika kata ya Tengelea Wilayani Mkuranga jana wakiwa kwenye mkutano Mkuu wa kijiji wamedai shamba lao la kijiji lenye ekari 12.5 ambalo linadaiwa limeuzwa kinyume na sheria na bwana Emmanuel Mwakambinga kwenda kwa Celina John Chanja tangu mwaka 2014.
Bwana Mohamed Maluyo Mkazi wa kijiji cha Hoyoyo anaelezea kwamba shamba hilo walikuwa wanatumia kama shamba la kijiji kwa kilimo tangu mwaka 1984-1985,hivyo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya afya wananchi walikubaliana wajenge zahanati ambapo baada ya kutaka kuanza utaratibu wa kujenga zahanati wakagundua kuna uzio umewekwa kwenye eneo la shamba hilo.
Siti Pazi anasema “kutokana na ukosefu wa huduma ya afya hapa kijiini inatugharimu hasa ukipata uchungu wakina mama tunajifungulia njiani lakini pia usafiri ni wa bodaboda ambao gharama yake kwa mwananchi wa kawaida hawezi kumudu ambao kwa pikipiki ni Tsh 6000 kwenda hospitali ya wilaya na kurudi.
Bi Siti aliongeza kwa kusema wanaomba haki itendeke ili kupata shamba la kijiji ili litumike kujenga zahanati kwani watapunguza changamoto wanazokutana nazo kwa kuwa mpaka sasa Mh Diwani ameshafanikiwa kupata mabati 100 na matofali 6000 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa zahanati hiyo.
Diwani wa Kata ya Tengelea Mh Shaban Manda anasema kwamba” baada ya kuona kuna mgogoro wa zahanati ya hoyoyo iliyojengwa na taasisi ya WAMA nikalisemea kwenye kikao cha baraza la madiwani ambapo ilipelekea kuundwaji wa kamati ili kufuatilia kuhusu zahanati hiyo lakini tuliambiwa kwamba zahanati sio ya kwetu”
Manda aliendelea kusema Katika kuhakikisha wanaitika wito wa kuwasaidia wananchi kwenye huduma ya afya halmashauri imeahidi kutoa matofali 6000 na bati 100 na Mh Abdallah Ulega ameahidi kutoa mifuko 100 ya saruji.
“Eneo hili ni la kwetu na tumekubaliana na wananchi wangu kushikamana pamoja kwakua wenzetu wanatumia nguvu ya fedha katika kufinya kupata haki yetu wananchi wa hoyoyo tunaonewa kwakua zahanati ya kwanza tuliikosa na sasa hivi wanasema shamba sio letu.”
Afisa Ardhi Mteule bwana Mussa Kichumu alisema ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashari ya Mkuranga ilipokea barua ya malalamiko tarehe 9/07/2018 kutoka kwa Mh Diwani wa kata ya Tengelea kuhusiana na uuzwaji wa ardhi ya kijiji kinyemela.
Kichumu alisisitiza kwamba kwakua sheria ya ardhi ya vijiji Na 5 ya mwaka 1999 imewapa mamlaka serikali ya kijiji juu ya usimamizi wote wa ardhi ya kijiji ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji iliamuandikia barua Ofisa Mtendaji wa kijiji cha hoyoyo barua ya tarehe 19/07/2018 ya kutaka kuwasilisha taarifa juu ya lalamiko hilo.
Kichumu aliongeza mpaka sasa wanaendelea kusubiri taarifa hiyo ili waone namna gani Halmashauri inaweza kuingilia kati na kutatua mgogoro huo kwa mujibu wa sheria.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.