Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mh Filberto Sanga amewataka wasichana kubadili tabia ili kujiepusha na maambukizi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 walioko shuleni na walio nje ya shule.
Mh Sanga aliyasema hayo leo hii kwenye hospitali ya Wilaya ya Mkuranga wakati wa uzinduzi wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi Kiwilaya ambapo inaenda sambamba na maadhimisho ya wiki ya chanjo ambayo inafanyika kila mwaka na utoaji wa chanjo ya sindano ya kuzuia polio kwa watoto wenye wiki ya 14.
Mh sanga aliongeza ili kujiepusha na Saratani ya mlango wa Kizazi inatakiwa wasichana wakiongozwa na wazazi wao kubadili tabia kwa kujiepusha na shughuli zenye kusababisha kwenda kinyume na maadili ya Mtanzania pia kujiepusha na ngono katika umri mdogo,kuepuka uvutaji wa sigara,kuepuka kubeba mimba katika umri mdogo na kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu.
Mratibu wa chanjo hiyo Bi Anna Liachema alisema dalili za saratani ya mlango wa kizazi ni kutokwa uchafu kwenye uke na majimaji uliopauka wa rangi ya kahawia au wenye damu, kutokwa damu bila mpangilio au kutokwa damu baada ya kujamiiana,maumivu ya miguu na kiuno na kuchoka,kupungua uzito pamoja na kupungukiwa na hamu ya kula.
Aidha aliongeza kwamba dalili mbaya zaidi zinazoweza kujitoeza ni pamoja na kuishiwa damu,figo kushindwa kufanya kazi na kupatwa na fistula na uvimbe wa tezi.
Swaumu Said mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mkuranga mwenye umri wa miaka 14 baada ya kupata chanjo alisema”sisikii maumivu yoyote baada ya kuchomwa sindano hivyo nawasihi wasichana wenzangu waje kupata chanjo ili kujikinga na saratani ya mlango wa kizazi kwani pia ni bure”.
Saratani ya Mlango wa uzazi ni mabadiliko ya ukuaji wa seli za mlango wa kizazi,mabadiliko ya ukuaji wa seli hizi husababisha misuli au viungo vingine mwilini kuathirika.
Saratani hii inaweza kusambaa na kuweza kushambulia kibofu cha mkojo,uke na sehemu ya chini ya utumbo mkubwa na baadaye figo,ini na sehemu zingine.
Mwaka 2017-2018 jumla ya wanawake 2791 walifanyiwa uchunguzi wa Saratani ya mlango wa kizazi kati yao 63 waligundulika na dalili za awali za saratani,60 walipatiwa matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Mkuranga na 3 walipewa rufaa kwenda Hospitali ya Ocean Road kwa matibabu zaidi.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.