Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani ikiongozwa na Kaimu Afisa Mipango Zawadi Aristites leo wamefanya ziara ya kukagua utekelezaji hatua za awali za ujenzi wa stendi ya mabusi ya kisasa iliyopo katika kata ya Mwandege Kijiji cha Kipala Wilayani humo.
Akizungumza katika ziara hiyo mratibu wa mradi ambaye pia ni mtumishi wa Halmashauri ya wilaya Mkuranga kutoka idara ya mipango Ndg. Sospeter Missian alisema mpaka kufikia sasa kamati iliamua kufanya utaratibu wa kumtafuta mzabuni kupitia kitengo cha manunuzi ambapo ilipatikana kampuni ya “IBRA CONSTRUCTION LTD” ambao walisaini mkataba wa kufanya kazi ya kusafisha na kusawazisha eneo kuanzia 2/4/2020 na mkataba huo unatekelezwa kwa siku (30) tangu tarehe ya makubaliano.
Katika uwasilishaji wa taarifa yake Ndg. Missian alisema kwa kiasi kikubwa kazi iliyofanyika ni kuondoa vichaka vyote vilivyokuwepo katika eneo hilo lenye ukubwa mita za mraba laki moja tisini na tatu elfu na sitini na saba (193,067) kulingana na vipimo vya wataalamu wa ardhi ni sawa na hekari (50) ila mpaka kufikia leo tarehe 29/5/2020 eneo lote limeonekana kuwa safi na taratibu za kusawazisha eneo bado zinaendelea ili kuipa sura ambayo walikubaliana katika mkataba wao wa kazi na mzabuni .
Sambamba na hilo Ndg. Missiani hakusita kuainisha changamoto zinazoikabili kazi hiyo ni pamoja na kutoonekana kwa alama za mipaka, kuharibika kwa baadhi ya vifaa vya buldoza ikiwemo kupasuka kwa “Hydrolic pipe” na kukatika kwa “ bolt” za chini na ajali ya kujeruhiwa kwa mwananchi na mashine wakati wa kazi.
Akijibu changamoto za kutoonekana kwa mipaka Afisa Mpimaji wa Ardhi Moses Makongoro alisema “ mawe ya mipaka (beacon) yalishapandwa isipokua zilikua zikingolewa lakini walikuja tena kuweka nondo kama alama lakini nazo ziling’olewa na buldoza wakati wa kusafisha eneo, hata hivyo mawasiliano yalifanyika na Mkuu wa kitengo cha upimaji wa Ardhi Wilaya ya Mkuranga Ndg. Issa Msenga na amesema mara baada ya kumaliza kusafishwa kwa eneo watarudishia alama kwa kuwa majira nukta (coordinate) ya eneo hilo wanazo.
Akihitimisha taarifa yake Mratibu wa mradi alisema jumla ya kiasi cha shilingi milioni arobaini na tisa laki sita na sabini na tisa elfu (49,679,000) pamoja na VAT zimetumika kama gharama za kusafisha eneo, ikiwemo ukodishwaji wa mashine, gharama za kuileta na kuirudisha mashine, gharama za gari ndogo iliyotumika kusindikiza mashine, mafuta za kuendeshea mashine hiyo pamoja na gharama za kumlipa aliyekua anaiendesha mashine.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.