Baraza la Madiwani Wilayani Mkuranga likiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mh.Juma Abeid jana limeazimia kuwachukulia hatua watendaji wote waliosimamia ujenzi wa nyumba za watumishi kuanzia hatua ya utafutaji wa eneo mpaka hatua ya ujenzi.
Azimio hilo lilitolewa wakati wa mkutano wa kawaida wa Baraza la madiwani lililofanyika hapo jana kwenye ukumbi wa kiguza flex ambapo ilionekana kuna changamoto juu ya uhamiaji kwenye nyumba za watumishi zilizopo eneo la Mkwalia Kitumbo kata ya Mkuranga zilizogharimu zaidi ya Milioni 300.
Akizungumza mbele ya Mkutano wa Baraza la Madiwani Afisa Utumishi na Rasilimali watu Wilaya bwana Valentine Mbai alisema”Ni kweli ilitakiwa mpaka mwezi julai mwaka huu watumishi wote waliopangiwa kuishi kwenye nyumba hizo wawe tayari wamehamia lakini kutokana na eneo hilo kuwa oevu ni vigumu watumishi kuhamia kwani ifikapo kipindi cha masika nyumba zote hujaa maji na hivyo huweza kuhatarisha usalama wa Mkuu wa idara husika”
Bwana Mbai aliongeza kuwa palipo na nyumba hizo kuna maji mengi hata walipoweka nguzo za umeme zilianguka na hali hiyo ilisababisha hata transifoma kulipuka na kuharibika.
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mh.Filberto Sanga alisema”Eneo limetafutwa, limejengwa hadi tunaazimia kuhamia leo hii mnakuja kusema si salama, inaumiza sana fedha ya Serikali inatumbukizwa kwenye ujenzi ambao hauna tija”
Mh Sanga aliendelea kusema kwamba hivi karibuni zimepelekwa fedha kwa ajili ya kuweka umeme ile hali eneo halifai kwa ajili ya makazi ya watu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mh.Juma Abeid alisema nyumba za watumishi zina zaidi ya miaka saba yeye akiwa diwani kwa kipindi hicho alipinga eneo hilo kujengwa nyumba za watumishi lakini alipuuzwa na viongozi wa juu yake.
Baraza la madiwani limeazimia kwa kuitaka Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iwachunguze na kuwachukulia hatua watumishi wa Halmashauri hiyo, walioruhusu kuidhinisha na kujengwa nyumba za wakuu wa idara katika eneo la mkondo wa maji ile hali haina sifa.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.