Watu sita wamejeruhiwa na wafugaji jamii ya wamang’ati kwa kupigwa na fimbo sehemu mbalimbali za miili yao ikiwemo kichwani baada ya wafugaji hao kuvamia kijiji cha Kondo Mwelanzi kilichopo katika kata ya Bupu Wilayani Mkuranga.
Akizungumza chanzo cha tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mh Filberto Sanga amesema sababu kubwa ni wafugaji ambao wametokea Wilaya ya Kisarawe kuingia katika kata hiyo kupitisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima, wakulima wakawaswaga ng’ombe hao na ndipo wafugaji takribani nane wakajiunga na kuwavamia wanakijiji hao na kuwapiga.
Sanga alisema kuwa wananchi waliopigwa wawili walikuwa si wakazi wa kijiji hicho bali ni wakazi wa Dar es salaam waliokwenda kutembelea ndugu zao na wengine ni wakazi wa kijiji hicho huku mmoja akiumizwa vibaya kichwani na kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Hatua ambazo tumechukua mpaka sasa mara baada ya kupata taarifa tulituma askari wetu kwenda kufanya kazi lile eneo lakini kwa bahati mbaya wale wafugaji walikuwa wameshakimbia msituni”Sanga alisema.
Sanga alisema katika kuhakikisha amani inakuwepo wametumia askari wetu kwenda eneo hilo kwa ajili ya uinzi na usalama ,naomba wananchi wawe watulivu na serikali inaangalia njia bora ya kutatua tatizo hilo ili kuhakikisha migogoro ya wakulima na wafugaji haitokei tena.
Wakati huo huo Sanga alikwenda kijiji cha Kondo Mwelanzi kuwafariji wananchi na kuwapa pole na kuwasihi kutojibu mapigano kwa aina yoyote ya silaha kwani serikali ipo pamoja nao na endapo itatokea dalili yoyote mbaya ajulishwe haraka ili hatua za haraka zichukuliwe.
Sanga aliongeza kwamba wale wananchi wote wanaoshirikiana na hao wafugaji wasitishe ushirikiano huo kwa kua hawana lengo zuri lakini pia watafutwe na endapo watabainika hatua kali za kisheria zichuliwe dhidi yao.
Kaimu Mganga Mfawidhi Wilaya ya Mkuranga Dkt. Ndaki Barnabas alisema mnamo Agosti 22 mwaka huu majira ya saa 4 usiku walipokea majeruhi watatu hali zao zikiwa mbaya na mmoja amekimbizwa hospitali ya Muhimbili kwa matibabu zaidi na wengine wamepatiwa matibabu wanaendelea vizuri.
Diwani wa kata ya Bupu Mh Abasi Msangule alisema tukio hilo limezua sintofahamu kwa wananchi hivyo kuomba serikali kulishughulikia suala la wafugaji ili kuepusha madhara zaidi.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.