Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu ( Uwekezaji ), Angellah Kairuki amewapongeza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga Mkoa wa Pwani kwa Kuwapokea na kuwalea vizuri wawekezaji sambamba na kuwataka kutenga maeneo ya uwekezaji na kuhakikisha wanaweka miundo mbinu stahiki ili kuongeza mapato ndani ya Wilaya hiyo.
Akiwa Wilayani Mkuranga jana kwa ziara ya siku mbili ya kutembelea baadhi ya viwanda, kwa lengo la kujionea shughuli mbali mbali zinazofanywa pamoja na changamoto wanazokumbana nazo, Kairuki amevipongeza viwanda hivyo kwa kuzaliza bidhaa bora sambamba na kulipa tozo zote za Serikali na kuvitaka baadhi ya viwanda ambavyo havijajiunga na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Kufanya hivyo ili wafaidike na fursa zinazopatika katika Taasisi hiyo.
Pamoja na hayo Waziri Kairuki amewaondoa shaka wawekezaji hao kwa kutoa ahadi ya kuzichukua baadhi ya changamoto ambazo zimeonekana ni kikwazo kikubwa na kuzifikisha katika maeneo husika ili zipatiwe ufumbuzi na hatimaye viwanda hivyo viendelee kufanya kazi kama ambavyo Raisi Dr. John Pombe Magufuli anavyotaka kwa maana ya kutekeleza Sera ya Viwanda.
Amesema pamoja na kuwasilisha hayo pia atawasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola kwa ajili ya kuona ni namna gani wataboresha jeshi la zima moto ndani ya Wilaya ya Mkuranga kwani viwanda vilivyopo ni vingi lakini kuna changamoto kubwa kwa jeshi hilo kwa kukosa vifaa vya kuzimia moto, hoja ambayo iliwasilishwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkuranga Ally Msikamo.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga amewataka wamiliki wa Viwanda kutowafungia milango Viongozi na Taasisi wezeshi na badala yake wanatakiwa kutoa ushirikiano ili kuendeleza mahusiano mema katika shughuli za uzalishaji mali kati ya Serikali na viongozi wa Viwanda hivyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga Kanyala Mahinda, ambaye pia ni Afisa Mipango amesema kwa Halmashauri hiyo inategemea mapato yake kupitia vyanzo vikuu viwili ambavyo ni madini ya mchanga na tozo kutoka viwandani ambapo kwa kipindi kilichopita 2018/2019 wamefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 1.5 na kuongeza kuwa kuna changamoto ya baadhi ya viwanda kulipa tozo katika Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam.
Viongozi wa viwanda wametakiwa kusaidia jamii inayowazunguka kwa kuchangia maendeleo mbalimbali katika sekta ya Elimu, Afya na nyinginezo kutokana na faida wanazopata katika bidhaa wanazotengeza katika viwanda hivyo.
waziri Kairuki katika ziara yake Wilayani Mkuranga ametembelea kiwanda cha Kubangua Korosho (Sabai), Kiwanda cha Tofali (Shafa), Kiwanda cha kutengeneza Vifaa vya umeme(Everwell) , vingine ni Kiwanda maji (Ice Drop), kiwanda cha Nondo (Lodhia ), kiwanda cha WAJA Mabati pamoja kiwanda cha Kuchakata samaki (Abajuko)
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.