Wakulima na Wafugaji Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani wametakiwa kutokubali kuingizwa katika Migogoro ya aina yoyote ile na hasa ile inayowahusu wao moja kwa moja, eidha iwe ya kisiasa au kimaslahi ya mtu au Kiongozi yoyote kwa kisingizio cha shughuli zao za kilimo na ufugaji, sambamba na kuwekwa miundo mbinu rafiki katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wafugaji.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina akiwa katika Mkutano maalumu uliohudhuriwa na Wakulima na Wafugaji katika kiwanja cha Ofisi ya Kijiji Kimanzichana Kusini, na kuwasisitiza wakiruhusu nafasi hiyo basi wasitarajie kupata maendeleo na hawatabaki salama.
Mpina akifafanua zaidi amesema kila mwananchi ana haki ya kuishi popote na kufanya shughuli zake bila kubughuziwa na mtu yoyote isipokuwa anatakiwa kufuata taratibu tuu, na kuwataka viongozi pamoja na wataalamu kutumia sheria ya fidia kumaliza migogoro hiyo ambapo Mkulima atawajibika kulipa gharama endapo atafanya uharifu kwa wanyama na wafugaji kulipa fidia kwa wakulima watakapofanya uharibifu katika mazao ya wakulima.
Amesema Mfugaji akilisha ng’ombe wake katika shamba la Mkulima basi alipe madhara hayo kama kwamba Mkulima amefikia kuvuna na Mkulima akimkata Ng’ombe wa Mfugaji basi nae alipe Ng’ombe mzima sambamba na kuwataka Viongozi wa Vijiji kutenga njia za kupitisha Mifugo wakati wa kwenda kulisha na zile zitakazotumika wakati wa kupeleka Mifugo mnadani ili kuondoa kero za mifugo kuharibu mazao ya Wakulima.
Waziri Mpina ametoa ahadi ya kutoa vifaranga 130,000 bure kwa wafugaji wa samaki baridi sambamba na kuhimilisha Ng’ombe 1000 bure, hii ikiwa ni jitihada za pamoja akishirikiana na Naibu Waziri wake Abdallah Ulega wakiwa na azma ya kuhakikisha wanafikia malengo ya Rais Dr. John Pombe Magufuli ya kuona kila mwananchi anapata fursa ya kujiongezea kipato.
Akiwasilisha taarifa fupi kwa Waziri Mpina, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde amesema Msitu wa Misangani ni changamoto kubwa kwa Wakulima na Wafugaji na hasa wafugaji ambao wanahama kutoka katika Wilaya nyingine kama Kisarawe na Kibiti.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga amesema suala la wakulima na wafugaji ni changamoto kubwa na hasa wale wafugaji ambao wanahama hama na kumuhakikishia Waziri kuwa wamekuwa wakitumia vikao na Mikutano mbalimbali katika kutatua migogoro hiyo.
Tarehe 21 mwezi huu waziri Mpina atatuma timu nyingine kwa ajili ya kuja kuona ni namna gani Migogoro hii inatokea ili kutafuta njia sahihi ya kumaliza Migogoro hii ndani ya Wilaya ya Mkuranga.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.