Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Juma Abeid ambaye ni Diwani wa Kata ya Magawa, amegawa viatambulisho vya msamaha wa matibabu kwa wazee 210 katika kata ya hiyo kwa lengo la kuvitumia kwa ajili kupata huduma ya Afya bure katika hospitali za Serikali.
Zoezi hilo amelifanya jana akiwa kwenye Mkutano maalumu wa kugawa vitambulisho hivyo na kusema Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga imetumia shilingi milioni 20 kutengeneza vitambulisho na kuwahakikishia wazee hao kuwa zoezi hili ni endelevu kwa Kata zote 25 ili kuhakikisha kila mzee aliyoko ndani ya Wilaya hii anapata kitambulisho hiko.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Neema Nyalusi amewataka wazee wote waliopata vitambulisho vya msamaha wa matibabu kuanza matibabu katika ngazi ya Zahanati zilizoko Vijijini hadi ngazi ya Wilaya sambamba na kuwahamasisha wazee hao wasikubali kuachiwa wajukuu ambao hawana vitambulisho vya Bima ya Afya.
Akiongea kwa kujiamini baada ya kupata Kitambulisho cha msamaha wa matibabu Fatuma Juma amewaomba Madaktari na Wauguzi kutoa huduma hiyo bila kuwanyanyasa pamoja na kuiomba Serikali kuruhusu vitambulisho hivyo kutumika kwenye huduma zote kwa maana ya kupatiwa vipimo pamoja na Dawa.
Katika kuhakikisha huduma hii inawafikia wazee wote, Juma avave ambaye pia ni mnufaika wa huduma hiyo amewataka wazee wote kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha kupata vitambulisho vya msamaha wa matibabu kwa wazee na hatimae kupata matibabu bure kwa kutumia vitambulisho hivyo.
Wilaya ya Mkuranga ni miongoni mwa Wilaya zinazotekeleza agizo la Raisi Dr. John Pombe Magufuli la kuhakikisha kuwa wazee wote wanapata Matibabu bure kupitia Vitambulisho hivyo vya Msamaha wa Matibabu.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.