Baraza maalumu la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga tarehe 29 Agosti 2024 limekaa kwenye Ukumbi wa Flex Garden n0a kujadili taarifa za fedha za Halmashauri kwa Mwaka wa fedha unaoishia 30 Juni 2024.
Miongoni mwa taarifa zilizowasilishwa ni pamoja na ile ya mapato na matumizi kwa Mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo Halmashauri ilikusanya kutoka vyanzo vyake vya ndani na vile vya ruzuku jumla ya shilingi Bilioni 67.9 na kutumia shilingi Bilioni 54.5 kwa matumizi ya mishahara na matumizi yote ya kawaida.
Akiwasilisha taarifa hiyo Mweka hazina wa Halmashauri hiyo Cornery Sima amesema fedha taslimu imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 3.3 Mwaka 2023 mpaka shilingi Bilioni 13.0 Mwaka 2024 ambayo imesababishwa na ongezeko la fedha za miradi ambayo fedha zake zilipokelewa mwishoni mwa Mwaka wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akichangia taarifa hiyo Adili Kinyenga Diwani wa Kata ya Mipeko amesema ufuatiliaji wa ulipaji wa kodi na ushuru wa Serikali uendelee kwa kuongezewa nguvu maeneo ya mijini ili kuweza kutekeleza miradi kwa ufanisi.
Nae Diwani wa Kata ya Kitomondo Zuberi Salum ameshauri kujitahidi kulipa madeni ya wadai ili kujenga imani na baadhi ya wananchi wanaofanya kazi za miradi mbalimbali na Halmashauri.
Akitoa Salamu za Serikali Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nassir Ali amewaomba Madiwani wote wilayani humo kuweka agenda ya Ulinzi na Usalama katika vikao vya maendeleo ya Kata WDC.
Amesema kukiwa na usalama katika maeneo hayo utawarahisishia wananchi kutekeleza miradi yao ya maendeleo kwa uhakika sambamba na kusimamia ufanyikaji wa Mikutano na vikao vya kisheria katika maeneo yao.
Aidha amewaomba kuhakikisha kila mradi unaofikishwa katika Kata zao wananchi wapate taarifa kamili za ujio wa miradi hiyo ili waweze kuchangia kutekeleza miradi hiyo.
Akifunga Mkutano huo Mwenyekiti wa Baraza hilo Mohamedi Mwela ameahidi kushirikiana na wataalam kwa kupitia vikao watafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali ili kuiwezesha Halmashauri hiyo kufanya vizuri.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.