Ofisi ya Afya kupitia kitengo cha Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na Mganga mkuu Halmashauri wilaya ya Mkuranga, imeendesha mafunzo elekezi kwa walezi na wamiliki wa vituo vya malezi kutwa (Day care Centres) ndani ya wilaya ya Mkuranga ili kutatua changamoto mbalimbali zinazovikabili vituo hivyo na watoto wanaolelewa katika vituo hivyo
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa ‘Resources Centre’ Kiguza Wilayani Mkuranga yalikua na lengo ya kutatua changamoto mbalimbali ikiwamo majengo wanayofundishia, walimu wanaofundisha pamoja na mbinu za kufundishia ili kupata muongozo na uelewa wa pamoja juu ya uendeshaji vituo hivyo
Akizungumza mara baada na mafunzo hayo Afisa Afya Mwandamizi, Bw. Elinas Jacob Nnko alisema, kama idara waliona iko haja ya kuendesha mafunzo hayo kwani miaka miwili iliyopita ndio kulianza kuwa na vituo hivi lakini tatizo ikawa wamiliki wengi kuwa hawajui namna sahihi ya kuendesha vituo hivyo na walikua hawajui miongozo kuhusiana na uendeshaji wa vituo vya watoto kutwa.
“ilikaa kamati ndogo ikishirikisha Afisa Afya, Afisa Ustawi wa jamii na wadau wengine ikajadili ikaona sasa iwakutanishe hawa wadau ili wawe na uelewa wa pamoja kuhusu vituo vya kulea watoto kutwa na maeneo ya makazi kwa watoto wanaoishi mazingira magumu ili sasa pale miongozo mbalimbali na serikali na wadau wanapotaka kutoa elimu tuwe na uelewa wa pamoja na tuwe tunaelewa nini maana ya vituo hivi” alifafanua Bw. Nnko.
Naye, Afisa Ustawi Halmashauri (W) Mkuranga Bi. Happyness Aloyce alisema, msukomo wa kufanya mafunzo hayo pia ulitokana na mkanganyiko uliokuwepo kwa wamiliki wa vituo kushindwa kutofautisha vituo vya malezi kutwa ‘Day Care Centres’ na shule za watoto ‘Nursery schools’, huku akipongeza muitikio mkubwa wa washiriki na kutoa wito kwa washiriki hao kwenda kuyafanya kwa vitendo yale waliyojifunza
Kwa upande wake Walter Meer, mshiriki kutoka shirika la ‘Marafiki wa Watoto’ linalojishughulisha na kusaidia watoto wenye saratani na mgongo wazi pamoja na kituo cha malezi ‘Mwanangu Day Care’, alishauri vituo vingine kuanza kujumuisha watoto wenye ulemavu na sio kuchukua watoto wasio na ulemavu pekee kwani bado kuna tatizo kubwa la watoto wenye ulemavu kufungiwa ndani
Aliongeza kuwa lengo la vituo hivyo ni kuandaa watoto kimalezi hivyo watoto wenye ulemavu wanahitaji fursa hiyo pia ambapo itawasaidia sana kujitambua na kupata ujuzi wa kimaisha ili waweze kujisaidia wenyewe kwa sasa na hata siku za usoni.
Vilevile Bi. Eliashukuru Tito ambaye ni mdhibiti Ubora katika Halmashauri Wilaya Mkuranga, alipongeza mafunzo hayo na kusisistiza washiriki kuzingatia suala la usafi na kuandaa maeneo rafiki ya michezo katika vituo vyao.
Mafunzo hayo yalifanyika kwa siku mbili ambapo mada mbalimbali zilitolewa kwa washiriki zikilenga zaidi kuboresha malezi ya watoto katika vituo hivyo
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.