Viongozi wa Vijiji na Kata ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani wametakiwa kupanga mikakati endelevu ya kutekeleza maagizo mbali mbali ya kitaifa yakiwemo ya kutunza Mazingira kwa kushiriki katika mazoezi ya upandaji Miti .
Akizungumza kwenye Baraza la Ushauri Wilaya (DCC) Mkuranga lililokutana leo kwenye ukumbi wa Flex Garden Kiguza, Mkuu wa Wilaya Mkuranga Filberto Sanga alitaja kuwa mambo hayo ni pamoja na upandaji Miti na kushiriki kikamilifu katika usafi wa kila jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Sanga akiiongoza Baraza hilo aliwataka Watendaji katika ngazi zote kuhakikisha miti yote ambayo inatarajiwa kutolewa bure na TFS Wilayani humo inapandwa maeneo yote mashuleni na maeneo binafsi kwa lengo la kutunza Mazingira kama alivyoagiza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo amesisitiza kufanya hivyo pamoja na kutunza kumbukumbu.
Kiongozi huyo pia aliwataka Madiwani na Watendaji wahamasishe wananchi katika maeneo yao kujitokeza kwa wingi katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura ambalo linatarajiwa kuanza Februari mwaka huu ili wananchi hao waweze kutumia haki yao kikatiba ya kushiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Aidha amesisitiza Watendaje wa Vijiji na Kata ambao ni walinzi wa amani kuhakikisha wanatimiza maadili ya kazi kwa kukaa kwenye vituo vyao vya kazi ili waweze kutoa huduma kwa wananchi kwa ukaribu zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mkuranga Mhandisi Mshamu Munde akijibu swali la mmoja wa wajumbe wa Baraza hilo amesema Halmashauri tayari wamepima eneo linalotarajiwa kujengwa Chuo cha Ufundi (VETA) katika Kijiji cha Shungubweni na wapo hatua za mwisho ya kupata hati lengo likiwa ni kuwaokoa vijana wanaokosa nafasi ya kujiunga na sekondari au kidato cha tano kukitumia chuo hiko sambamba kufaidika na uwepo wa Viwanda.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wametakiwa kuwachukulia hatua za kisheria vyama vyote vya msingi (AMCOS) ambavyo wameshindwa kurudisha fedha hadi sasa baada ya kuwadhulumu wakulima wa Korosho msimu uliopita.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.