Baraza la Madiwani linalouunda Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani limeazimia kuundwa kwa Kamati maalum itakayoshughulikia kero Migogoro ya Mipaka sambamba na baadhi ya Viwanda ambavyo vinazalisha bidhaa Wilayani humo lakini Kodi za Huduma wanalipa Dar es salaam.
Akizungumza kwenye Baraza hilo lililofanyika jana katika ukumbi wa Flex Garden Mkuranga, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na uvuvi Abdallah Ulega ameweka bayana mkakati huo wa ufuatiliaji wa kina umelenga Viwanda vyote (86) vilivyopo ndani ya Halmashauri hiyo vilipe ushuru hatimaye waweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashari hiyo, Mhandisi Mshamu Munde amesema tume hiyo ambayo itakuwa na mchanganyiko wa baadhi ya Madiwani na wataalam itashughulikia Migogoro ya Mipaka inayohusisha Wilaya za Kibiti, Kisarawe, Ilala na Kigamboni kwa kukutana na Waziri mwenye dhamana William Lukuvi na kumuomba kufika Mkuranga ili kusaidiana nae na hatimaye kumaliza Mgogoro huo.
Akitoa salamu za Serikali Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga amewataka Madiwani kuchukua Tahadhari katika kipindi hiki cha Mvua kuwa mabalozi wazuri katika Kata zao kuwaeleza wananchi wawe makini wanapovuka mito inayopitisha Maji sambamba na kuwazuia watoto wa shule hadi hapo hali itakapokuwa sawa.
Na katika kuhakikisha Ujenzi wa Kituo kikubwa cha polisi wilaya ya Mkuranga kinakamilika baada ya kusimama kwa Muda, Madiwani wa Baraza wamemtaka Mkuu wa Polisi Wilayani humo kuandaa bajeti na kuiwasilisha kwao ili waweze kuendelea kuchangia ujenzi huo.
Akifunga kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri Juma Abeid aliwaomba Madiwani wenzake kutumia muda uliobaki kabla ya uchaguzi Mkuu kusimamia pesa zinazotumwa kwenye Kata zao zinalingana na ubora wa Miradi husika.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.