1.UTANGULIZI
Kilimo, ubanguaji na masoko ya zao la korosho Tanzania husimamiwa na Sheria ya Tasnia ya Korosho Na. 18 ya mwaka 2009 (sura ya 203 ya Sheria za Tanzania) pamoja na Kanuni zake za mwaka 2010 (Tangazo la Serikali Na. 420 la mwaka 2010). Sheria na Kanuni zinaweka masharti ya msingi kwa ajili ya kuzingatiwa na mkulima, mnunuzi, mbanguaji na wadau wengine wa korosho ili kuhakikisha kuwa korosho inayozalishwa, kununuliwa na kubanguliwa hapa nchini inakidhi ubora unaokubalika kimataifa ili kuiwezesha kupata soko la uhakika. Sheria pia inalenga kwa upande mwingine kumhakikishia mlaji au mtumiaji wa bidhaa za korosho ili aweze kupata korosho ambayo ina ubora wa uhakika.
Mwongozo unaweka na kufafanua utaratibu mzima wa usimamizi wa mauzo/masoko ya korosho kwa lengo la kutoa ufanunuzi wa masharti ya msingi yaliyomo katika Sheria na Kanuni za Korosho. Utaratibu huo ni katika ukusanyaji wa korosho kwenda kwenye maghala ya mnada, uhakiki wa ubora wa korosho, ununuzi wa korosho, malipo kwa wakulima, utoaji wa taarifa za mauzo, usafirishaji wa korosho ndani na nje ya nchi na usuluhishi wa migogoro ya mauzo/masoko kwa kuzingatia masharti yaliyomo kwenye Sheria na Kanuni za Tasnia ya Korosho
2.TOZO ZILIZOONDOLEWA KWENYE MJENGEKO WA BEI
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2016/2017,ilifuta baadhi ya ada na tozo ambazo zimeonekana kuwa kero kwa wananchi na kikwazo katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini.
Kwa mujibu wa Makadirio hayo, katika zao la korosho, tozo 5 kati ya 9 zilizokuwepo kwenye mjengeko wa Bei wa mwaka 2015/2016 zilifutwa rasmi.
Tozo hizo ni:-
I.Kusafirisha koroshoshilingi 50/= kwa kilo,
II.Gharama ya Mtunza ghala shilingi 10/= kwa kilo,
III.Ushuru wa Chama Kikuu cha Ushirika shilingi 20/= kwa kilo,
IV.Kikosi kazi kwa ajili ya ufuatiliaji wa zao la korosho shilingi 1/= kwa kilo na
V.Makato ya unyaufu.
Tozo na makato yaliyobakizwa msimu wa 2016/2017 ni:-
I.Ushuru wa Chama cha Msingi Shilingi 50/= kwa kilo,
II.Ushuru wa Halmashauri ya Wilaya asilimia 3-5 ya bei elekezi kwa kilo,
III.Mchango wa Mfuko wa Kuendeleza Zao la Korosho Shilingi 10/= kwa kilo,
IV.Magunia na kambashilingi 56/= kwa kilo.
Aidha kwa msimu wa 2017/2018 Serikali kupitia mkutano mkuu wa wadau wa Tasnia ya korosho uliofanyika mwezi Mei, 2017 mjini Dodoma, imeondoa tozo ya magunia na kamba Shilingi 56/= kwa kilo.
Serikali pia imefuta tozo ya leseni ya dola 1,000 kwa wanunuzi wa korosho wanaosafirisha nje ya nchi na shilingi 1,000,000/= kwa wanunuzi wanaobangua nchini. Lengo kuu la Serikali la kufuta tozo hizo ni kuwafanya wanunuzi watoe bei nzuri kwenye minada na hivyo kuongeza kipato kwa wakulima.
3.MAGUNIA NA KAMBA
Mahitaji ya magunia kwa wakulima ni 250,000. Hatua za uagizaji wa magunia (status) kwa Chama Kikuu cha Ushirika (CORECU) ni kwamba magunia 83,000 yalikuwa tayari ghalani na magunia 167,000 yameshafika bandari ya Dar es Salaam na mchakato wa kuyatoa unaendelea.
Magunia yote yatakayotumika kuhifadhi korosho msimu wa 2017/2018, yatawekewa alama maalum ya utambulisho kwa kutumia rangi tofauti kwa kila chama kikuu cha ushirika na kwa upande wa CORECU rangi ya gunia itakuwa kijani.
4.UTARATIBU UTAKAOTUMIWA NA WAKULIMA KUKUSANYA NA KUUZA KOROSHO KWENYE MNADA MSIMU WA 2017/2018.
4.1 Maghala ya Mnada
Maghala ya vyama vya msingi na yaliyojengwa na miradi ya Serikali yatakayokidhi vigezo ikiwa ni pamoja na vyama vikuu vya ushirika na watu binafsi, mapya na yaliyotumika misimu iliyopita yatatumika kupokea na kuhifadhi korosho za wakulima kwa ajili ya mnada.
4.1.1Uendeshaji na Ugharamiaji wa Maghala ya Mnada
Mwendesha ghala atalipwa shilingi 25/= kwa kilo kutoka kwa mnunuzi, kama alivyolipwa msimu wa 2016/2017. Aidha kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za ghala, mwendesha ghala atatakiwa kupokea, kuzitunza na kuzitoa korosho zikiwa katika ubora na uzito kama alivyozipokea.
5.USAFIRISHAJI WA KOROSHO KUTOKA CHAMA CHA MSINGI HADI GHALA LA MNADA.
Vyama vya msingi kwa kushirikiana na Maafisa Ushirika wa
wilaya watatakiwa kukokotoa gharama halisi ya kusafirisha korosho husika kwa kuzingatia umbali halisi kati ya chama cha msingi husika na ghala la mnada. Aidha kwa vyama vya msingi vyenye vyombo vya usafiri vinashauriwa kuwa wabunifu kwa kutumia vyombo hivyo ili kuwapunguzia wakulima gharama ya kusafirisha korosho zao. Gharama zitakazokokotolewa zitalipwa na wakulima husika.
6.MGAWANYO WA MAJUKUMU
Ufanisi wa Mfumo wa Mauzo katika zao la korosho utategemea ushirikiano baina ya wahusika ambao watakuwa chini ya usimamizi wa Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na mkoa husika.
6.1 Mkulima
I.Kutambua umuhimu wa kufungua akaunti benki kwa ajili ya kupokelea fedha zake za malipo ya korosho.
II.Kuvuna, kukausha, kuchambua na kudarajisha korosho zake kwa mujibu wa sheria na kanuni za Tasnia ya korosho hapa nchini.
III.Kupeleka korosho zilizodarajishwa katika kituo cha kukusanyia cha Chama cha msingi.
IV.Kupokea hati ya kupokelea korosho zake katika chama cha msingi (GRN) ikionesha uzito wa korosho na daraja.
V.Kushiriki kwenye mnada wa mauzo ya korosho.
VI.Kufuatilia taarifa za mauzo ya korosho zake kwenye chama cha msingi.
VII.Kuuza korosho zake kwenye Mfumo rasmi badala ya kangomba.
VIII.Kuweka kumbukumbu sahihi za mauzo ya korosho zake.
6.2 Chama cha Msingi
I.Kuhakikisha kabla ya msimu wa ununuzi wa korosho kuanza, kuandaa mzani unaotumika kupimia korosho katika ghala lake unakaguliwa na kuthibitishwa na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) chini ya sheria ya vipimo na mizani hapa nchini.
II.Kupokea korosho zilizodarajishwa kutoka kwa mkulima huhakiki uzito kwa kuzipima kwa mzani uliokaguliwa na kuthibitishwa na Wakala wa Vipimo Tanzania na kuziweka katika magunia mapya ya kitani (Jute) au katani (Sisal) yenye viwango vya ubora vilivyothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuhakiki ubora wake.
III.Kutoa GRN (Hati ya kupokelea) kwa kiasi cha korosho na ubora aliopkea kutoka kwa mkulima.
IV.Kutunza korosho za Mkulima na ubora wake na kuhakikisha kuwa uzito halisi wa korosho ni kilo 80 kwa kila gunia kabla ya kupeleka kwenye ghala la mnada lililo karibu yake kwa ajili ya mauzo.
V.Kuandika jina la chama chake na namba ya utambulisho iliyotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania katika kila gunia la korosho.
VI.Kuweka kumbukumbu sahihi za GRN katika rejesta itakayosainiwa na mkulima.
VII.Kupeleka korosho katika Ghala la mnada kwa kutumia hati ya kusafirisha korosho inayotolewa na AMCOS (PDN) ya chama cha msingi), Chama kikuu (Agizo la kutoa korosho-Order) na Halmashauri ya wilaya (Kibali cha kusafirisha korosho kwenda ghala la mnada).
VIII.Kupokea hati ya kupokelea korosho katika ghala la mnada (WHR).
IX.Kuwasilisha hati ya kupokelea korosho (WHR) na Hati ya Ubora wa korosho zilizopokelewa ghala la mnada kwa chama kikuu.
X.Kufuatilia taarifa za mauzo na malipo ya korosho za chama chake.
XI.Kuweka kumbukumbu sahihi za mauzo ya korosho za chama chake.
6.3 Mwendesha ghala la mnada
I.Kupokea korosho zilizodarajishwa kutoka chama cha msingi.
II.Kuhakikisha kuwa korosho zinafungashwa kwenye magunia ya katani (sisal) au kitani (jute) ambayo ni mapya na yamethibitishwa na TBS na kuwekewa alama ya utambuzi ya Bodi ya Korosho Tanzania.
III.Kuhakikisha magunia yana alama ya chama cha msingiitolewayo na Bodi ya Korosho Tanzania.
IV.Kuhakikisha kuwa idadi ya magunia ya korosho anayopokea yanaendana na idadi ya magunia yaliyotoka chama cha msingi na yana uzito wa korosho wa kilo 80 kila moja.
V.Kuhakikisha kuwa korosho ni kavu na zina unyevu usiozidi asilimia kumi (10 %).
VI.Kupokea na kuhakiki nyaraka za kutolea mzigo
VII.Kupima uzito wa korosho wakati wa kutoa ghalani.
VIII.Kutunza na kuzitoa korosho kwa mnunuzi husika zikiwa katika ubora na kiasi kama alivyozipokea kutoka kwa chama cha msingi. Kiwango kisichozidi 0.5 % cha unyaufu wa korosho kinaweza kutokea endapo korosho itakaa ghalani kwa muda wa miezi 6 na kuendelea.
IX.Kutoa taarifa ya mapokezi na uondoshaji wa korosho kwa Chama Kikuu cha Ushirika.
X.Kutoa taarifa ya mauzo na malipo kwa Bodi ya Korosho Tanzania.
6.4 Halmashauri ya wilaya.
I.Kuelimisha na kuhamasisha wakulima kuhusu mfumo wa Stakabadhi Ghalani.
II.Kuhakiki ubora wa korosho kupitia wataalamu waliopatiwa mafunzo na Bodi ya korosho kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele.
III.Kuhakikisha wakulima wanapata malipo stahiki kutokana na mauzo ya korosho zao.
IV.Kudhibiti ununuzi holela wa korosho maarufu kama ‘ Kangomba/Chomachoma’.
V.l kwanza na/au daraja la pili na kuzipanga katika loti tofauti kwa kuzingatia madaraja hayo.
7.UHAKIKI WA UBORA WA KOROSHO GHAFI
7.1 Mtunza ghala atatakiwa kuajiri mhakiki wa ubora wa korosho aliyefuzu
mafunzo na kupata cheti kutoka Bodi ya Korosho Tanzania kuanzia mwaka 2014/2015 na kuendelea.
7.2 Mtunza ghala atatakiwa kuwa na vifaa vya uhakiki wa ubora wa korosho
vilivyopitishwa na Bodi ya Korosho Tanzania ambavyo ni kipima unyevu (moisture meter), mikasi ya kukata korosho, na mzani mdogo wa kidigitali unaopima uzito kuanzia kilo moja (1).
7.3 Mnunuzi akishakabidhiwa korosho alizonunua mnadani atawajibika
kulinda na kuhifadhi ubora wa korosho hizo hadi anaposafirisha au anapobangua.
7.4 Mnunuzi aliyeshinda mnada na kulipia korosho husika endapo atahitaji
kujiridhisha ubora wa korosho alizozilipia kabla ya kuziondosha kutoka ghala la mnada, atatakiwa kutoa taarifa kwa maandishi kwa meneja wa mtunza ghala husika. Mhakiki wa ubora wa korosho wa mtunza ghala ndiye atakayehakiki ubora wa korosho hizo mbele ya mnunuzi husika.
7.5 Endapo kutatokea mgogoro wa ubora wa korosho zilizo ghala la mnada,
wahusika wa mgogoro watatakiwa kuitaarifu Bodi ya Korosho Tanzania kwa maandishi ndani ya siku mbili ili iweze kutuma jopo la wataalam kuthibitisha ubora wa korosho hizo ambapo matokeo ya uhakiki wao yatakuwa ya mwisho.
8.UNUNUZI WA KOROSHO GHAFI
8.1 Mfanyabiashara atakayehitaji kununua korosho ghafi katika msimu
husika atatakiwa awe na Leseni itakayotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania kwa ajili hiyo.
8.2 Mnunuzi mwenye leseni ya kununua korosho iliyotolewa na Bodi ya
Korosho Tanzania katika msimu husika atatakiwa kununua korosho chini ya Mfumo wa Stakabadhi Ghalani.
8.3 Mnunuzi atatakiwa kuzingatia Sheria ya Tasnia ya Korosho Na. 18 ya
Mwaka 2009, Kanuni zake za Mwaka 2010, na Mwongozo Na. 1 wa Mauzo ya Korosho Ghafi katika msimu husika.
8.4 Mnunuzi atatakiwa kuzingatia masharti na vigezo vya mnada wa mauzo
ya korosho kama yalivyotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania katika msimu husika.
8.5 Mnunuzi atatakiwa kuwasilisha taarifa ya ununuzi wa korosho kila mwezi
kwa Bodi ya Korosho Tanzania akionesha kiasi alichonunua, alichosafirisha nje ya nchi na thamani yake kwa bei ya malipwani (FOB price) na/au kiasi alichobangua ndani ya nchi na thamani yake.
8.6 Mnunuzi atakayehitaji kwa sababu yoyote ile, kuhamisha umiliki wa
korosho alizozinunua kwenye mfumo rasmi atatakiwa kuomba idhini kwa maandishi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, atapatiwa PDN mpya baada ya kurejesha zile za awali toka kwa mnunuzi mwingine - PDN hizo zitawasilishwa Makao Makuu au Matawini ili zitolewe mpya.
9.MALIPO KWA WAKULIMA
9.1 Vyama vya msingi vinatakiwa kukusanya korosho kutoka kwa wakulima
bila kuchukua mkopo benki. Mrajisi wa vyama vya Ushirika asimamie utekelezaji wake.
9.2 Wakulima watastahili kulipwa fedha zote za malipo ya korosho husika
kwa mkupuo mmoja kupitia akaunti zao za benki kulingana na bei halisi ya korosho zao kwenye mnada husika baada ya kutoa tozo za mjengeko wa bei na wao wenyewe kutoa gharama halisi za usafirishaji wa korosho kwenda ghala la mnada.
9.3 Malipo kwa mkulima yatafanyika kupitia Benki Akaunti iliyosajiliwa kwa
jina lake.
9.4 Vyama vikuu vya Ushirika viandae “sales Catalogue” kulingana na jinsi
korosho zilivyoingia ghalani; Korosho za kwanza kuingia ghalani ziwe za kwanza kuuzwa (FIFO)
9.5 Ni marufuku kwa vyama Vikuu na vya msingi kuchelewesha malipo ya
wakulima au kuwalipa wakulima kwa kuchanganya minada. Malipo yote yafanyike ndani ya siku saba (7) toka siku mnunuzi alipoingiza fedha za malipo ya mnada husika kwenye akaunti ya pamoja ya chama kikuu husika.
10.UENDESHAJI WA MINADA YA KOROSHO
10.1 Kamati ya mauzo ya korosho katika msimu husika itaundwa na Bodi ya
Korosho Tanzania. Kamati hiyo itahusisha wafuatao;
Menejimenti ya Bodi ya korosho
Sekretarieti ya Mkoa
Chama Kikuu cha Ushirika
Vyama vya Ushirika vya Msingi
Mrajis Msaidizi wa Mkoa
Wakulima na
Wenyeviti wa Halmahauri
10.2 Mwenyekiti wa kamati hiyo atatokana na wajumbe wa kamati.
Mameneja wa vyama Vikuu vya ushirika watakuwa Makatibu wa kamati hizo chini ya usimamizi wa Bodi ya korosho.
10.3 Korosho zote za wakulima zilizokusanywa katika maghala ya mnada
zitauzwa kwa mnada isipokuwa pale litakapotokea tatizo katika maghala ya mnada au uchache wa korosho, Bodi ya Korosho Tanzania itatoa maelekezo.
10.4 Uamuzi wa kuuza korosho kwa mnunuzi ni wa wakulima kupitia minada
husika.
10.5Chama cha msingi kitatakiwa kuwasilisha stakabadhi (Wareheouse
Receipt), fomu iliyojazwa orodha ya wakulima na hati ya ubora wa korosho zilizopokelewa katika ghala la mnada kwa chama kikuu husika.
10.6 Kila mnunuzi atatakiwa kuweka kinga ya zabuni kwa fedha taslimu (Bid
Security) katika Akaunti ya Bodi ya Korosho kwa viwango vifuatavyo:-
TANI KWA MNADA KIASI (TSHS)
50 - 500100,000,000.00
501 - 1000300,000,000.00
1001 - nakuendelea500,000,000.00
10.7Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikianan na Vyama Vikuu vya Ushirika
wataandaa ratiba itakayoonyesha tarehe na mahali pa kufanyia minada na kuwatangazia wadau.
10.8Kila mnunuzi atatakiwa kuwasilisha na kusajili zabuni yake iliyofungwa
kwa lakiri (Seal) kwenye sanduku la zabuni lililopo sehemu ya mnada husika kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana.
10.9Taarifa ya mshindi wa mnada itatangazwa na Bodi ya Korosho Tanzania
kwenye mnada na itawekwa kwenye tovuti ya Bodi ya Korosho Tanzania (www.cashew.go.tz) mara tu baada ya mnada.
10.10Kila chama kikuu cha Ushirika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
au Mkuu wa Wilaya husika watatakiwa kuhakikisha usalama wa sanduku la zabuni muda wote.
10.11 Kila chama kikuu kitatakiwa kusafirisha sanduku la zabuni hadi kwenye
kituo cha mnada katika wilaya husika kwa mujibu wa ratiba itakayotolewa na Bodi ya Korosho Tanzania.
10.12 Kila Chama Kikuu cha Ushirika kitatoa Hati ya Madai (Sales Invoice) na
kumpa mnunuzi pale pale kwenye mnada au ndani ya saa 24 baada ya mnada. Afisa Ushirika Msimamizi wa eneo husika kwa kushirikiana na mjumbe wa Bodi ya korosho watasimamia zoezi hilo. Viongozi na watendaji wa vyama vikuu vya ushirika wanatakiwa kwenda kwenye minada wakiwa na nyaraka zote za mnada husika ili kurahisisha uandaji na utoaji wa invoice ndani ya muda ulioelekezwa kwenye Mwongozo huu.
10.13 Mnunuzi atatakiwa kulipia korosho kupitia Benki ndani ya siku 4 baada ya
siku ya mnada.
10.14 Mnunuzi atatakiwa kulipia kwa mujibu wa ankara ya mauzo (Sales
invoice) iliyosajiliwa na Bodi ya Korosho Tanzania.
10.15 Mnunuzi hatapewa agizo la toleo (Release Warranty) na chama kikuu
husika mpaka akamilishe malipo yote kwa ankara ya mauzo husika.
10.16 Mnunuzi hatoruhusiwa kushiriki mnada unaofuata iwapo atakuwa
hajakamilisha malipo ya mnada uliopita.
10.17 Mnunuzi atatakiwa kukamilisha malipo stahiki ndani ya siku nne (4) za kazi
tangu tarehe ya mnada husika. Endapo mnunuzi atakuwa hajakamilisha
malipo, korosho husika zitanadiwa tena kwenye mnada unaofuata, na
mnunuzi husika kinga ya dhamana zabuni yake (Bid Security) itachukuliwa
(forfected) na hatoruhusiwa kushiriki minada inayofuata katika msimu huo.
10.18 Kila mjumbe wa kamati ya mauzo atatakiwa kusaini makubaliano ya
mauzo ya siku husika kuthibitisha kuwa mauzo yamefanyika kwa kuzingatia taratibu za mauzo kama zilivyowekwa na Bodi ya Korosho Tanzania.
10.19 Mauzo yoyote ya korosho yatakayofanywa nje ya utaratibu nje ya
Mwongozo huu yatakuwa batili na waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Korosho Na. 18 ya mwaka 2009 na Kanuni zake za mwaka 2010.
10.20 Kila Chama Kikuu kitauza korosho kwenye mnada, ni marufuku kuuza
korosho ambazo hazijatangazwa kwenye Sales Catalogue ya mnada husika.
10.21 Kabla ya mauzo, Chama Kikuu cha Ushirika kitatakiwa kutoa taarifa ya
malipo ya korosho zilizonunuliwa katika mnada uliotangulia na atasaini nyaraka ya taarifa hiyo.
11.UTOAJI WA TAARIFA ZA MAUZO YA KOROSHO
11.1 Bodi ya Korosho Tanzania itatoa taarifa za mwenendo wa soko la
korosho kila wiki kipindi cha msimu wa ununuzi wa korosho ghafi kupitia vyombo vya habari ikiwemo redio za kijamii zilizopo katika Halmashauri zinazolima korosho, na tovuti ya Bodi ya Korosho Tanzania (www.cashew.go.tz).
11.2 Mrajisi Msaidizi wa Mkoa atawajibika kutoa taarifa kwa Amcos na Bodi ya
Korosho kuhusu mauzo ya korosho.
11.3 Kila chama cha msingi kitatakiwa kubandika taarifa za mauzo ya
korosho za wakulima wake kwenye mbao za matangazo za chama chake.
12.USAFIRISHAJI WA KOROSHO GHAFI NDANI YA NCHI
12.1 Mnunuzi atatakiwa kusafirisha korosho kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi
saa 12:00 jioni.
12.2 Mnunuzi atatakiwa kusafirisha korosho kwa kutumia PDN inayotolewa na
Bodi ya Korosho Tanzania.
13.UTOAJI WA NYARAKA ZA UNUNUZI NA USAFIRISHAJI WA KOROSHO
13.1Bodi ya Korosho Tanzania ndiyo chombo pekee hapa nchini chenye
mamlaka ya kutoa kibali cha kusafirisha korosho zilizonunuliwa na Mnunuzi kutoka kwenye Mfumo rasmi uliokubalika kutumika katika mwaka husika, iwe ndani ya nchi au nje ya nchi.
13.2 Huduma za kiofisi kwa wasafirishaji wa korosho itatolewa bure na Bodi ya
Korosho Tanzania kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:30 jioni Jumatatu hadi Ijumaa isipokuwa siku za mapumziko kuanzia saa 2:00 asubushi hadi 7:00 mchana.
13.3 Huduma za kutoa PDN kwa upande wa maghala ya mnada ni kuanzia
saa 1:30 asubuhi hadi saa 11:30 jioni Jumatatu hadi Jumapili.
13.4 Hati za kusafirisha korosho itolewe kwa korosho zilizonunuliwa kwenye
minada tu.
14.NAMNA YA KUGHARAMIA SHUGHULI AMBAZO TOZO ZAKE ZIMEFUTWA
14.1 Gharama za uendeshaji maghala ya mnada zitalipwa na mnunuzi
ambazo ni shilingi 25/= kwa kilo wakati wa kuondosha korosho zao mara baada yakukamilisha malipo kwa korosho husika kulingana na Mwongozo wa Bodi ya Leseni za Maghala.
14.2 Maafisa ushirika wa wilaya, viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi
na vyama vikuu kwa kuwashirikisha wakulima wao wakokotoe na kuridhia gharama halisi za usafirishaji wa korosho kwenda maghala ya mnada kwa kuzingatia umbali halisi. Gharama hizo zilipwe kutokana na maelekezo ya Mrajisi wa vyama vya ushirika Tanzania.
14.3 Kila mshiriki wa mnada atajigharamia.
14.4 Kwa msimu wa 2017/2018, Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania,
Itagharamia magunia na kamba. Menejimenti ya Bodi ya Korosho itatoa mwongozo wa namna ya utekelezaji.
15.USULUHISHI WA MIGOGORO
15.1 Endapo kutatokea malalamiko ya upande mmoja kutuhumu
kutotendewa haki na upande mwingine mlalamikaji atatakiwa kuwasilisha malalamiko yake kwa maandishi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania ndani ya siku 14 tangu tarehe ya tukio.
15.2 Bodi ya Korosho Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Tasnia ya Korosho Na.
18 ya mwaka 2009 na Kanuni zake za mwaka 2010 itaitisha kikao cha usuluhisi ndani ya siku 21 kwa ajili ya kujadili na kutoa maelekezo ya namna ya kumaliza jambo husika.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.