“Nyinyi wote ni wachunga na mtaulizwa kwa vile mlivyo vichunga”, haya ni maneno yaliyotamkwa na Mh. Abdallah ulega, Naibu waziri wa mifugo na uvuvi na Mbunge wa Jimbo Mkuranga Mkoa wa Pwani wakati akilihutubia Baraza Maalumu la Madiwani liiloketi leo katika ukumbi wa Flex Garden kwa dhumuni la kujadili masuala ya kinidhamu.
Ulega alitamka maneno hayo kwa lengo la kuwakumbusha waheshimiwa madiwani ya kuwa lengo lililowaweka katika kiti hiko kwa kipindi chote cha miaka mitano ni kuwaongoza na kuwahudumia wananchi wa Mkuranga katika kuwaletea maendeleo na kutimiza ahadi walizoziahidi kwa wananchi kabla ya kuwa madiwani, hivyo basi amewataka wale watakaorudi tena, warudi kwa lengo la kufanya kazi kwa weledi ili kuipeleka mbele Wilaya ya Mkuranga kwa kuwa dhamana ya maendeleo ipo mikononi mwao, “ninafahamu weledi wenu na uchapakazi wenu nendeni mkafanye kazi”alisisitiza
Aidha, Naibu waziri hakusita kumpongeza pia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mhandisi Mshamu Munde pamoja na watendaji wake wote kwa kuonesha ushirikiano wa dhahiri na kufanikisha baadhi ya miradi mbali mbali iliyoanishwa wilayani hapo lakini amemtaka Mkurugenzi kuendelea kusimamia yale yote ambayo wanayaacha kwa kipindi chote watakachokua katika harakati za uchaguzi na kumtaka kusimamia vyema bila kujisahau kwa kuwa wao hawatakuwepo…
Mh. Ulega aliona mbali zaidi kwa kusema wananchi wa Mkuranga wanaakili zao timamu wanaelewa walikotoka waliko na wanakotaka kwenda hivyo hata wanapoenda kuwania nafasi mbali mbali wajitathimini wakijua watu wanaowaomba dhamana ya uongozi ni wenye uelewa na wenye upeo chanya wa kutaka kuona maendeleo yanafanyika na sio maneno mengi kama ilivyozoeleka, alisisitiza “tuchape kazi hiyo ndo njia pekee itakayofanya tuendelee kuaminika na wananchi waliotupa dhamana ya kuwaongoza’….
Sambamba na hilo Mhandisi Munde alilihakikishia baraza hilo tukufu la madiwani akisema “tutasimamia yale yote ambayo yanatakiwa kuendelea kufanyika kwa kipindi chote ambacho hamtakua pamoja nasi na yale yote mliyoyazungumza tunayaunga mkono na tutayaendeleza kwa uadilifu”.
Baraza la madiwani linatarajiwa kufikia ukomo mapema mwezi huu kwa kuzingatia tamko la Waziri wa TAMISEMI Mh. Selemani Jaffo…
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.