Wakulima wa Vijiji vya Bupu, Panzuo na Chamgoi Wilayani Mkuranga wameshauriwa kutumia uwepo wa wafugaji katika vijijini vyao kama fursa ya maendeleo na sio kuwaona kama maadui hali inayopelekea kuwa na migogoro ya mara kwa mara
Akiongea katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijijini hivyo, Katibu Mkuu chama cha wafugaji Tanzania Ndg. Magembe Makoye ambaye pia ni mjumbe kamati ya usuluhishi migogoro kati ya wakulima na wafugaji nchini Tanzania, alisema, wakulima ndani ya vijiji hivyo hawana budi kuanza kuchukulia uwepo wa wafugaji katika maeneo hayo kama fursa ambayo itawapatia kipato kwa kufanya shughuli / biashara zinazohusisha mifugo hiyo
“Vijana wa Chamgoi tuanze kujiuliza kwanini wenzetu wafugaji wana pesa mwaka mzima? Basi tuiangalie hiyo kama fursa, mifugo ni pesa! Kama una eneo la ekari kadhaa unaweza kulizungushia na kukodisha kama eneo la malisho kwa wafugaji, hiyo ni pesa tayari” alisisitiza bwana Makoye
Aliongeza kwa kuwashauri wafugaji kufuata taratibu sahihi za kuingia katika vijiji hivyo ili waishi kwa mfumo sahihi tofauti na sasa wanavyojitenga hali inayohatarisha maisha yao, akitolea mfano wajawazito wa jamii hizo kujifungua katika mazingira magumu kwani wako mbali mno na vituo vya afya.
Jitihada hizi za kutatua migogoro hii zimekuja baada ya kuibuka mapigano kati ya wakulima na wafugaji mwishoni mwa mwaka jana ambapo kuliibuka mapigano kati ya wakulima na wafugaji jamii ya wamang’ati na ndipo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na Mbunge wa Mkuranga Mh Abdallah Hamis Ulega kumuagiza katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuunda timu ya wataalam ambao watashughulikia mgogoro kati ya wakulima na wafugaji katika Mkoa wa Pwani.
Kamati hiyo inayohusisha wajumbe kutoka wizara mbalimbali ikiwamo Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya makazi, Wizara ya Mambo ya ndani , Wizara ya Kilimo na Mifugo pamoja na Ofisi ya Rais inashirikiana na idara ya Kilimo na Mifugo pamoja na Idara ya Maliasili (Misitu) Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kufanya ziara maeneo yenye migogoro kati ya wafugaji na wakulima ili kupata suluhu ya pamoja
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.