Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Abdallah Ulega ambae pia ni Mbunge wa Mkuranga amewataka wataalam wa Afya ya Mifugo kusimamia sheria ya magonjwa ya wanyama Na.17 ya mwaka 2003 na kanuni zake ili kuimarisha udhibiti wa magonjwa nchini na kuwezesha biashara ya mifugo na mazao yake ili kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.
Mh ulega aliyasema hayo hapo jana wakati alipomuwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh luhaga Mpina kwenye maadhimisho ya siku ya Veterinari Duniani yaliyofanyika wilayani Mkuranga kwenye ukumbi wa upashanaji habari kiguza.
Akiongea mbele ya wananchi na wadau wa Mifugo Ulega alisema kazi za taaluma ya veterinari ni pamoja na kusimamia ukaguzi wa mazao ya mifugo kutoka shambani mpaka mezani kwa lengo la kuhakikisha usalama wa mazao kwa walaji na kudhibiti magonjwa ya wanyama ambayo yamendelea kupunguza tija katika uzalishaji.
Mh Ulega aliongeza kwamba ili kuhakikisha magonjwa ya mifugo yanadhibitiwa,Serikali katika mwaka 2017/2018 ilitoa waraka wa kudhibiti magonjwa ya mifugo.
Aidha alisisitiza kwamba waraka huo unazielekeza Serikali za Mitaa nchini kuwa na mipango endelevu ya udhibiti wa magonjwa kumi ya kipaumbele ambayo ni homa ya mapafu ya ng'ombe,ugonjwa wa miguu na midomo,kichaa cha mbwa,ugonjwa wa kutupa mimba,mdondo,kimeta,sotoka ya mbuzi na kondoo,mapele ngozi,homa ya mapafu ya mbuzi pamoja na magojwa tokezi kama vile homa ya bonde la ufa,Ndigana kali pia ilipendekezwa kuingia kwenye orodha ya kuudhibiti ugonjwa huu.
wakati huu huo Mh ulega aliahidi kutoa chanjo zenye thamani ya 1,200,000 kwa ajili ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ng'ombe baada ya mwakilishi wa wafugaji bwana Alolo Ngamnoni kuelezea juu ya wanyama wao wanavyokufa kutokana na ugonjwa huo na changamoto ya upatikanaji wa chanjo hiyo na gharama zake kuwa kubwa sana.
Dkt.Furaha Mramba Mtendaji Mkuu wa wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania katika Wizara ya Mifugo na uvuvi alisema ugonjwa wa mapafu unasambaa sana kutokana na kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine wanyama wenye ugonjwa huu huambukiza wenzao.
Dkt Mramba aliongeza kwamba dawa za homa ya mapafu zina gharama kubwa kwa sababu zinaletwa na watu binafsi"lakini chanjo hii ipo kwenye hatua za mwisho ili izalishwe hapa nchini na chanjo hii itafanyiwa majaribio hapa Mkuranga"alisema Dkt.Mramba
Siku ya Veterinari huadhimishwa siku ya Jumamosi ya Mwisho wa Mwezi Aprili kila mwaka kwa lengo la kukumbuka huduma ambazo zimekuwa zikitolewa na taaluma hii kwa jamii takriban miaka 50 iliyopita.
Mwaka huu imeangukia 28 April,2018 ila yameadhimishwa hapo jana.
Tanzania kama mwanachama wa Shirika la Afya ya Wanyama Duniani(OIE) inaungana na mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku hii muhimu.
kauli mbiu ya mwaka huu ni"Umuhimu wa taaluma yaVeterinari katika kuboresha maisha,usalama na uhakika wa chakula na maendeleo endelevu"
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga
Postal Address: P. O. Box 10, Mkuranga, Pwani, Tanzania
Telephone: +255232110038
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@mkurangadc.go.tz; ded.mkuranga@pwani.go.tz
Copyright ©2023 MkurangaDc. All rights reserved.